Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, tarehe nne Jamadul-Awwal ni kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zainab (s.a), shujaa wa Karbala. Wilaya ya Takwini ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa mada zinazozua tofauti katika mijadala ya itikadi, katika makala ifuatayo kwa kuchunguza mtazamo unaohusishwa na Mawahabi na kutolea ushahidi ripoti zilizomo katika vitabu vya Al-Buldan cha Ibn al-Faqih na Al-Ihtijaj cha Tabarsi, patachunguzwa tukio la ukimya wa watu wa Kufa kabla ya Bibi Zainab (s.a) kutoa hotuba yake.
Miongoni mwa fadhila ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu huwajaalia watu wema ni uwezo wa kufanya baadhi ya mambo katika ulimwengu, hii ina maana kwamba Mawalii wa Mwenyezi Mungu, kwa fadhila na idhini ya Mola wao, wanaweza kufanya baadhi ya mambo katika ulimwengu wa uumbaji na mahali. Katika historia yote, kuna mifano mingi inayoonesha kuwa watu wema wamefanya tasarruf katika mambo ya Takwini. Kwa mfano, Mashia na Ahlus-Sunna wamepokea kisa kuhusu Bibi Zainab al-Kubra (s.a), ambacho kinathibitisha Wilaya yake ya Takwini, makala hii inakizungumzia kisa hicho.
Kuthibitisha “Wilaya ya Takwini” ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu kwa kutolea ushahidi sehemu ya maisha ya Bibi Zainab (s.a)
Utangulizi
Miongoni mwa fadhila ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu huwajaalia watu wema ni uwezo wa kufanya tasarruf katika ulimwengu, kwa maana hiyo, Mawalii wa Mwenyezi Mungu wanaweza, kwa fadhila na idhini ya Mola wao, kufanya baadhi ya mambo katika ulimwengu wa uumbaji na mahali.
Tasarruf ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu katika ulimwengu ni miongoni mwa mambo ambayo Mawahabi wanayapinga, kiasi kwamba wanaichukulia itikadi ya kuamini jambo hilo kuwa hairuhusiwi, hali hiyo ni pamoja na kwamba katika historia kuna mifano mingi inayoonesha tasarruf ya watu wema katika mambo ya Takwini.
Kwa mfano, Mashia na Masunni wamepokea kisa kuhusu Bibi Zainab al-Kubra (s.a), kinachothibitisha Wilaya ya Takwini ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu, katika sehemu zinazofuata, pamoja na kueleza mtazamo wa Mawahabi kuhusu suala la Wilaya ya Takwini ya watu wema, tutaeleza pia mfano wa Wilaya ya Takwini ya Bibi Zainab (s.a), ambapo imesimuliwa na wanazuoni na wanahistoria wa madhehebu zote mbili.
Kutokuruhusiwa kuamini Wilaya ya Takwini kwa mtazamo wa Mawahabi
Katika itikadi ya Uwahabi, Wilaya ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu juu ya ulimwengu wa uumbaji na mahali ni jambo lisilowezekana. Kwa hiyo, kuamini kwamba watu wema wanaweza kufanya tasarruf katika mambo ya Takwini ni jambo lisiloruhusiwa. Kama tunavyosoma katika kitabu cha Fatawa za Kamati ya Kudumu (Fatawa al-Lajnah ad-Daimah), imeelezwa hivi:
«وأما التبرک بالصالحین الأحیاء فبدعة....وقد یکون شرکا أکبر إذا اعتقد فی الصالح أنه ینفع ویضر بتصرفه، وأنه یتصرف فی الکون ونحو ذلک»
Ama kutabaruku kupitia watu wema walio hai, hilo ni bid'a (uzushi katika dini).... Na wakati mwingine jambo hilo linaweza kuwa shirki kubwa, ikiwa mtu ataamini kwamba mtu mwema anaweza kuleta manufaa au kusababisha madhara kwa njia ya tasarruf yake, na kwamba anaweza kufanya tasarruf katika ulimwengu wa uumbaji na mambo yanayofanana na hayo.”
Katika kauli hii, inaonekana wazi kwamba kwa mujibu wa imani ya Mawahabi, kutafuta baraka kupitia watu wema, ambako wanakuchukulia kuwa ni bid'a, kunakuwa shirki kubwa ikiwa kutaambatana na kuamini Wilaya ya Takwini ya watu hao wema.
Hata hivyo, dai hili linatolewa licha ya kwamba katika historia kuna matukio mengi yanayoonesha kuwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu wamefanya tasarruf katika ulimwengu. Kwa mfano, Bibi Zainab (s.a) ni miongoni mwa watu wema ambao Mashia na Ahlus-Sunna wamesimulia tukio la tasarruf yake katika ulimwengu wa uumbaji na mahali, tukio hilo linaelezwa katika sehemu inayofuata.
Sehemu ya Wilaya ya Takwini ya Bibi Zainab (s.a)
Baada ya tukio la Ashura na kuuawa kishahidi Imam Hussein (a.s) pamoja na maswahaba wake waaminifu, jeshi la Umar Sa'd liliwateka nyara watu wa familia ya Mtume Mtukufu (saww). Mji wa Kufa ulikuwa kituo cha kwanza walikofikishwa watu wa familia tukufu ya Sayyidush-Shuhada (a.s).
Miongoni mwa matukio muhimu yaliyotokea katika mji wa Kufa ni hotuba ya kipekee ya Bibi Zainab (s.a). Katika tukio hilo, akiwa mbele ya Ibn Ziyad na watu wa Kufa, Bibi Zainab (s.a) alitoa hotuba yenye maudhui mazito kwa ujasiri na uthabiti wa moyo wa kupigiwa mfano.
Bila kuzingatia hata sifa nyingi ambazo wanazuoni wa Kiislamu wamempa kutokana na namna alivyotoa hotuba hiyo [2], jambo ambalo mwandishi analolizungumzia katika makala hii ni kudhihirika dalili fulani ya Wilaya ya Takwini ya Bibi Zainab (s.a) kabla ya kuanza hotuba hiyo.
Kama wanazuoni wa madhehebu zote mbili wanavyothibitisha: Wakati Hazrat Zainab (s.a) alipotaka kutoa hotuba katika mji wa Kufa, alifanya ishara ili ukimya utawale katika kikao hicho. Mara tu baada ya kufanya ishara hiyo, ukimya wa ajabu ulitawala kiasi kwamba hata kengele zilizokuwa zikining'inia kwa ngamia ziliacha kutoa sauti na kutulia.
Abu Abdullah Ahmad bin Muhammad al-Hamadani, anayejulikana kwa jina la Ibn al-Faqih, ambaye alikuwa mwanazuoni wa Kisunni wa karne ya nne Hijria, anaandika katika kitabu chake Al-Buldan, Wakati Bibi Zaina (as) alipotaka kutoa khutba yake:
«وقد أومأت إلی الناس أن انصتوا. فارتدت الأنفاس وسکنت الأجراس، ثم قالت: الحمد لله والصلاة علی نبیه»
“Wakati Hazrat Zainab (s.a) alipotaka kutoa hotuba, aliwaashiria watu wanyamaze na wasikilize. Mara tu baada ya kufanya ishara hiyo, pumzi zilikwama vifuani mwa watu na hata kengele zikatulia na kuacha kutoa sauti. Kisha akasema: ‘Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, na rehema zimshukie Mtume Wake.’”
Katika kitabu cha Al-Ihtijaj, kilichoandikwa na marehemu Tabarsi (r.a), tunasoma pia:
«فَأَوْمَتْ زَیْنَبُ بِنْتُ عَلِیِّ بْنِ أَبِی طَالِبٍ (علیهم السلام) إِلَی النَّاسِ بِالسُّکُوتِ قَالَ حِذْیَمٌ الْأَسَدِیُّ لَمْ أَرَ وَ اللَّهِ خَفِرَةً قَطُّ أَنْطَقَ مِنْهَا کَأَنَّهَا تَنْطِقُ وَ تُفْرِغُ عَلَی لِسَانِ عَلِیٍّ (علیه السلام) وَ قَدْ أَشَارَتْ إِلَی النَّاسِ بِأَنْ أَنْصِتُوا فَارْتَدَّتِ الْأَنْفَاسُ وَ سَکَنَتِ الْأَجْرَاس»
“Zainab, binti wa Ali bin Abi Talib (a.s), aliwaashiria watu wanyamaze. Hidhyam al-Asadi alisema: ‘Wallahi, sijawahi kumwona mwanamke mwenye staha na haya, lakini wakati huohuo mwenye uwezo mkubwa wa kuzungumza kuliko yeye. Alikuwa akizungumza kana kwamba anatoa maneno kutoka katika ulimi wa Ali (a.s). Alikuwa amewaashiria watu wanyamaze na wasikilize, ndipo pumzi zikakwama vifuani mwao na hata kengele zikatulia na kuacha kutoa sauti.’”
Katika riwaya hii pia imethibitishwa wazi kwamba baada ya Bibi Zainab (s.a) kufanya ishara, pumzi za watu zilikwama vifuani mwao na hata kengele za ngamia ziliacha kutoa sauti.
Kwa hiyo, inabainika kutokana na ripoti za kihistoria zilizopokewa na wanazuoni wa madhehebu zote mbili kwamba, kwa ishara na fadhila ya Bibi Zainab al-Kubra (s.a), hata kengele za ngamia ziliacha kutoa sauti na ukimya wa kupigiwa mfano ukatawala katika kikao hicho. Jambo hili linaonesha wazi Wilaya ya Takwini ya Bibi huyo mtukufu.
Inafaa kutajwa kwamba kuthibitisha Wilaya ya Takwini ya watu wema hakutegemei tu ushahidi uliotajwa hapo juu. Bali, wanazuoni wengi wa Kiislamu pia wamethibitisha wazi uwezekano wa jambo hilo.
Kwa mfano, Dawud bin Suleiman Naqshbandi, mwanazuoni wa madhehebu ya Shafi'i wa karne ya kumi na tatu Hijria, amethibitisha kwamba; Mawalii wa Mwenyezi Mungu waliofariki dunia wanaweza kufanya tasarruf [5]. Aidha, anaamini kwamba karama za watu wema hazikomei katika maisha ya dunia hii pekee, bali wanaweza pia kudhihirisha karama mbalimbali katika ulimwengu wa Barzakh. [6]
Jambo la kuvutia zaidi ni kwamba Ahmad bin Siddiq al-Ghumari, mwanazuoni wa Kisunni wa zama za karibuni ambaye hakuwa akimfuata mwanazuoni mwingine katika masuala ya kielimu kwa namna ya taqlid, pia ameeleza wazi jambo hili kwa kusema:
«وکان سید الدباغ رحمه الله من الاولیاء، ... و کنا مره فی دار بعض الاخوان و هو جالس بجنبی و خطر لی خاطر عظیم فی شانه، فانحنی علی یدی یقبلها من غیر سبب، و ذلک امام الناس، فعلمت ان ذلک تنازل منه و تواضع لاجل الخاطر الذی خطر لی فی شانه و کان و هو بفاس یرسل الی و انا بطنجه یخبر بامور غریبه و یقول: انا معک بین المرقعه و النعال»
“Sayyid al-Dabbagh, Mwenyezi Mungu amrehemu, alikuwa miongoni mwa Mawalii wa Mwenyezi Mungu.... Niliwahi kuwa pamoja na watu wengine katika nyumba ya mmoja wa ndugu zetu wa kidini, naye alikuwa ameketi kando yangu. Wakati huo, wazo kubwa kuhusu cheo na utukufu wake lilinijia akilini mwangu. Alisoma wazo lililokuwa akilini mwangu, kisha akainama na kuibusu mikono yangu bila sababu yoyote iliyoonekana, mbele ya watu. Hapo nilitambua kwamba alifanya hivyo kwa kujishusha na kuonesha unyenyekevu, kutokana na wazo lililonijia kuhusu cheo chake, ili nisije nikazidisha fikra za kumtukuza kupita kiasi.
Pia, alipokuwa katika mji wa Fez, alikuwa akinitumia ujumbe mimi nikiwa katika mji wa Tangier, akiniarifu kuhusu mambo ya ajabu na kusema: ‘Mimi niko pamoja nawe, katikati ya vazi la viraka na viatu.’”
Tija:
Kinyume na dai la Mawahabi, ambao hata kuamini Wilaya ya Takwini ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu wanakuchukulia kuwa ni jambo lisiloruhusiwa, ushahidi unaopatikana katika simulizi za kihistoria unaonesha kwamba Mawalii wengi wa Mwenyezi Mungu walikuwa na Wilaya ya Takwini.
Kama wanazuoni wa madhehebu zote mbili walivyothibitisha wazi, Bibi Zainab (s.a), katika kikao kilichofanyika katika mji wa Kufa, kwa ishara na fadhila yake, aliweza kuwafanya waliokuwapo wanyamaze, wakiwemo viumbe wengine waliokuwa wakitoa sauti.
Kwa hiyo, kwa mujibu wa hoja zilizotolewa katika makala hii, Wilaya ya Takwini ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu ni jambo linaloweza kuthibitishwa kwa ushahidi, na hivyo kuamini jambo hilo hakuna tatizo.
Maoni yako